Breaking News

KIFO CHA MR. EBBO... KILICHOMUUA CHAJULIKANA


Abel Loshilaa Motika a.k.a Mr Ebo enzi za uhai wake.
Na Joseph Ngilisho, Arusha
VILIO, majozi na huzuni, bado vimelizunguka Jiji la Arusha kufuatia kifo cha staa mkubwa wa muziki wa Kizazi Kipya Bongo mwenye ladha ya asili ya kabila la Wamasai, Abel Loshilaa Motika a.k.a Mr Ebo (37), aliyefariki usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita, Desemba, Mosi mwaka huu.

NINI KIMEMUUA?
Swali lililokuwa likizunguka, lilihoji ni nini kilichomuua Mr. Ebbo aliyekuwa amelazwa kwa muda katika Hospitali ya Mission iliyopo nje kidogo ya Jiji la Arusha, Usa River wilayani Arumeru angali bado akipendwa na mashabiki wake?

UPUNGUFU WA DAMU NI UGONJWA GANI?
Kwa mujibu wa kaka wa marehemu aliyezungumza na The Biggest IQ Paper, Ijumaa Wikienda katika boma la Motika maeneo ya Masai Camp, Moshilaa Motika, mdogo wake alisumbuliwa na upungufu wa damu mwilini kwa muda mrefu.

NI ANEMIA AU LEUKEMIA?
Gazeti hili liliwadodosa madaktari bingwa juu ya hali hiyo kiafya ambapo magonjwa yanayosumbua wengi hivi sasa ya Anemia na Leukemia yalitajwa.

CHANZO CHA IJUMAA WIKIENDA
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Mr. Ebbo amekuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa huo ambapo alikuwa akiishiwa damu, lakini cha kushangaza, muda mfupi baada ya kuongezewa nyingine, bado hali ilibaki vilevile.

DAMU ILIKUWA INAKWENDA WAPI?
Chanzo hicho kilidai kuwa ilifika wakati hata madaktari wakawa wanashangaa damu inakwenda wapi kufuatia hali ya kuongezewa nyingine, lakini vipimo vikaonesha kama hajaongezewa chochote.

Baba wa marehemu.

DAMU YAPELEKWA NJE YA NCHI
Ilidaiwa kuwa katika harakati za kupigania uhai wa Mr. Ebbo aliyetamba na kibwagizo cha ‘Mi Mmasai Bana’, madaktari walifikia hatua ya kupeleka damu yake nje ya nchi kwa ajili ya vipimo, lakini wataalam waligonga mwamba.

AHAMISHIWA ARUSHA
Habari zilizidi kudai kuwa baada ya hali kuzidi kuwa mbaya, alihamishiwa Arusha kwani baadhi ya ndugu walidhani kinachosababisha aumwe ni mazingira ya Jiji la Tanga alikokuwa akiishi na kuendesha shughuli zake ikiwemo studio yake ya muziki ya Motika Records.

Kaka yake marehemu.

Hata hivyo, pamoja na jitihada zote hizo ndani na nje ya nchi, Mr. Ebbo aliyekuwa amejipanga vilivyo kwenye gemu alitangulia mbele ya haki.

ARUSHA YAZIZIMA
Baada ya kutangazwa kwa kifo cha Mr. Ebbo ambaye ukiwa umekasirika na ukasikia wimbo wake lazima ucheke, Jiji la Arusha lilizizima kwa majonzi huku msanii huyo akikumbukwa zaidi kwa vichekesho vyake.

Mdogo wake marehemu.

KUZIKWA LEO
Mr. Ebbo atazikwa leo katika boma la Motika maeneo ya Masai Camp Moshono, nje kidogo ya Jiji la Arusha yakitanguliwa na misa maalumu ya kuuombea mwili wa merehemu katika Kanisa la Lutheran lililopo Kata ya Olorieni.

HISTORIA
Mr Ebbo alikuwa mtoto wa 10 kati ya watoto 11 wa mzee Loshilaa Motika (85), ambapo kati yao wawili ni marehemu akiwemo Mr. Ebbo ambaye ameacha mke na watoto watatu.

KUTOKA IJUMAA WIKIENDA
Mungu ametoa na Mungu ametwaa, jina lake lihimidiwe. Rest In Peace Mr. Ebbo!

No comments