Breaking NewsNa Joseph Ngilisho, Arusha
GALACHA katika Muziki wa Bongo Fleva, Abel Losholaa Motika ‘Mr. Ebbo’ aliyefariki dunia Alhamisi Desemba Mosi, mwaka huu, saa 5:30 usiku katika Hospitali ya Misheni iliyopo Usa River, jijini hapa ameagwa na kuzikwa juzi Jumatatu, Risasi Mchanganyiko linaripoti kwa simanzi tele.

Msanii huyo ambaye pia alikuwa mtayarishaji wa muziki huo katika Studio za Motika Records za jijini Tanga, alizikwa katika makaburi ya Boma la Motika, Masai Camp Moshono, mjini hapa.

Mr. Ebbo amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kukaukiwa damu na maji mwilini, hali iliyosababisha kila mara kuongezewa, lakini viliendelea kukauka.

Katika maziko hayo, mamia ya waombolezaji walionekana kujawa na simanzi nzito walijitokeza katika eneo hilo kwa ajili ya kumuaga mpendwa Mr. Ebbo.
ATOLEWA HOSPITALINI KWA MSAFARA
Majira ya saa 2:30 asubuhi, msafara mkubwa kutokea Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mt. Meru alipokuwa amehifadhiwa, ulianza kuelekea nyumbani kwa marehemu.

Watu wengi walijitokeza katika msafara huo, ambapo walijipanga barabarani wakionekana kuwa na majonzi mazito kutokana na msiba huo uliofanya Arusha kuzizima na kuwa kimya kabisa kwa siku nzima ya Jumatatu.

Barabara za East Afica, Mkuu wa Mkoa, Boma na Kijenge ambazo ndizo msafara huo ulipopita wakati ukielekea nyumbani kwa marehemu zilijaa watu tangu mapema asubuhi wakisubiri kuagana na rafiki Mr. Ebbo.

AAGWA KWA SAA TATU
Kutokana na umati mkubwa wa watu uliojitokeza nyumbani kwa marehemu kwa lengo la kuuaga mwili wake, ilichukua zaidi ya saa tatu kwa shughuli hiyo na bado watu hawakumalizika.

Shughuli ya kuaga ilianza saa 4.00 asubuhi, ikabidi saa 7:15 isitishwe kutokana na wingi wa watu waliondelea kumiminika na kuunga foleni ya kwenda kutoa heshima zao za mwisho.

VILIO VYATAWALA
Kelele za mayowe zilisikika kina kona katika eneo lote wakati wa shughuli za kuagwa, baadhi ya watu walizidiwa na kupoteza fahamu wakati na baada ya kutazama mwili wa marehemu.

Wakati ndugu, jamaa na marafiki wakipita mbele ya jeneza lenye mwili wake, nyimbo zake mbalimbali zilikuwa zikisikika hasa ule wa Mi Mmasai kupitia spika zilizokuwa kila kona ya eneo hilo.

MISA YA MAREHEMU
Ibada ya misa ya kumuombea marehemu Mr. Ebbo ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Olorieni na kuongozwa na Askofu wa Kanisa hilo, Dayosisi ya Arusha, Thomas Laiser.

Askofu Laiser aliwataka watu kuwa na upendo hasa katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa Mr. Ebbo kwa kuwa upendo ni ishara njema ya kumkumbuka marehemu.

FAMILIA
Wazazi wa marehemu Mr. Ebbo walionekana kuwa watulivu sana muda wote wa shughuli za maziko ya mtoto wao mpendwa, kadhalika mkewe na wanawe watatu walionesha huzuni lakini walijikaza na kuwa wavumilivu.

Aidha, kaka, dada na ndugu wengine wa karibu walionesha ustahimilivu katika tukio hilo la kihistoria la kuagana na mpendwa wao waliyeishi naye kwa miaka 37 ya uhai wake.

WASANII WASUSA
Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, wasanii maarufu wa Bongo Fleva hawakuonekana katika msiba huo zaidi ya Fred Maliki ‘Mkoloni’ ambaye ni Memba wa Kundi la Wagosi wa Kaya aliyekuwa kwenye maziko hayo.

Mkoloni aliyefika jijini hapa akitokea Tanga, muda wote alionekana mwenye huzini kuu, alipopita mbele ya jeneza lenye mwili wa marehemu alishindwa kujizuia na kuangua kilio.
“Nitamkumbuka Mr. Ebbo kwa mengi, hasa uwezo wake wa ubunifu aliokuwa nao. Medani ya muziki imepoteza mtu muhimu sana,” alisema Mkoloni muda mfupi kabla hajapita mbele ya jeneza la mwili wa marehemu.

WAHESHIMIWA
Wanasiasa waliohudhuria maziko hayo ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Mazingira Batilda Burian, Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Godbless Lema, Mbunge wa zamani wa jimbo hilo Felix Mrema na  Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Goodluck Ole Medeye.

Lema alisema: “Mr. Ebbo alikuwa msanii wa aina yake, atakumbukwa kwa mengi.
Cha muhimu ni kushika yale mema na kuyaendeleza, hapo tutakuwa tumemuenzi vyema.”

Marehemu Mr. Ebbo alizaliwa Mei 26, 1974 katika Hospitali ya Mkoa ya Mt. Meru ya jijini hapa, ameacha mke na watoto watatu wa kike.

KUTOKA RISASI MCHANGANYIKO
Hakuna maneno mepesi ya kueleza jinsi tulivyoguswa na msiba huu mzito. Tunajua kwamba familia ya marehemu ipo katika wakati mgumu sana, lakini tunawaomba wajipe moyo.

Kikubwa kwetu ni kumuombea ili apate mapumziko mema. Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe. – Amina.

No comments