Breaking News

KANUMBA ALIPANGA KUJENGA SHULE......SINTAH ASEMA KANUMBA ALIONEKA MWENYE HASIRA SANA KABLA YA KIFO CHAKE..........


 

Katika hatua nyingine, Fidelis Butahe na Pamela Chilongola wanaripoti kuwa mchaguaji maeneo ya kupigia picha za filamu za msanii Kanumba, Rahim Khatib alisema marehemu Kanumba alinunua eneo la ekari 15 huko Mpiji mkoani Pwani kwa ajili ya ujenzi wa shule yake ya sekondari.

Khatib alisema Kanumba alikuwa na mpango huo muda mrefu na kwamba lengo lake lilikuwa kuwasaidia wanafunzi wa eneo hilo ambao hutembea muda mrefu kutokana na shule kuwa mbali na eneo hilo.

 “Kanumba alikuwa na mipango mizuri katika maisha yake, kuna eneo kubwa alilonunua Mpiji ili ajenge shule ya sekondari,” alisema Khatib.

Alifafanua kuwa hadi anafariki dunia, aliacha kiasi cha fedha zaidi ya Sh 40 milioni katika Kampuni yake ya Kanumba The Great.

“Marehemu ameacha fedha zaidi ya Sh 40 katika kampuni yake, magari matatu na hivi karibuni alinunua jingine aina ya Toyota Land Cruiser, ”alisema Khatib.

Katika hatua nyingine Khatib alisema kifo cha Kanumba ni pigo kwa watu waliokuwa wakifanya naye kazi akiwemo yeye mwenyewe kwa kuwa walikuwa wakimtegemea kwa kiwango kikubwa.

Sintah naye alonga

Kwa upande wake msanii maarufu wa filamu nchini, Christina Manongi maarufu kama Sintah ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa kwanza kufika nyumbani kwa marehemu Kanumba muda mfupi baada ya msanii huyo kuanguka, alisema kuwa siku tano kabla ya Kanumba kufariki, alikuwa na hasira tofauti na alivyomzoea.

Sintah ambaye alikuwa na msanii huyo katika Viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam Jumapili ya Aprili mosi pamoja na mwigizaji mwingine, Steve Nyerere alisema kuwa kila alichokuwa akimuuliza Kanumba, alimjibu kwa ukali.

“Ni tofauti na nilivyomzoea, siku ile ya Jumapili tulikaa pale Leaders Club mpaka usiku sana na kila jambo nililokuwa nikizungumza naye alinijibu kwa mkato na ukali kweli, ilinishangaza,” alisema Sintah

Alifafanua kuwa moja ya mambo waliyokuwa wakizungumza na Kanumba ni pamoja na yeye kutaka kuacha uigizaji, suala ambalo marehemu Kanumba hakuliunga mkono na kumjibu kwa ukali kuwa asijitoe katika uigizaji.

No comments