Breaking News

KAJALA AMPOKEA LULU KWA VILIO SEGEREA

Na Waandishi Wetu
JUMATANO iliyopita vilio vilitanda ndani ya Gereza la Segerea, Dar baada ya msanii wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja (pichani) kusikia mwigizaji mwenzake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ naye ameingizwa ndani ya  selo hilo maarufu, ni Ijumaa pekee linaloweza kunyetishia habari hiyo kwa kina.
KAJALA AMPOKEA KWA KILIO
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani, Kajala ambaye alifikishwa Segerea mwezi uliopita akituhumiwa kutakatisha fedha haramu, alijikuta akiangua kilio pale aliposikia Lulu kaingizwa gerezani hapo.
Chanzo hicho kilidai kuwa kama vile haitoshi, Lulu naye aliangusha kilio alipoambiwa Kajala yupo gerezani na kuwafanya mahabusu wengine kuacha shughuli zao na kumkodolea macho staa huyo anayetamba katika sinema za Kibongo.
Lulu alifikishwa gerezani hapo baada ya mchana wa siku hiyo kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu na kusomewa tuhuma zake baada ya kusota kwa muda mrefu katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay .
SIRI YA  KUFIKISHWA MAHAKAMANI
Mpango wa kumfikisha mahakamani Lulu ulifanywa kwa siri kubwa ili kuwakwepa mapaparazi wasiweze kunasa na kufuatilia habari za msanii huyo ambaye Watanzania wana shauku ya  kujua hatma yake.
Awali, ilisemekana kuwa Lulu alikuwa afikishwe katika Mahakama ya Kinodndoni jijini Dar lakini baada ya wahusika kusikia kuwa mapaparazi walishanasa taarifa hizo  na kujazana mahakani hapo, haraka wakaamua kubadilisha mwelekeo na kumpeleka Kisutu.
Ilisemekana kuwa kingine kilichowafanya wahusika kutomfikisha Lulu katika Mahakama ya Kinondoni ni kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

HAKUWEKWA MAHABUSU
Wakati Lulu akipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu hakuwekwa katika mahabusu ya mahakama hiyo kama ulivyo utaratibu wa watuhumiwa wengine wanapofikishwa hapo pindi wanaposubiri kusomewa tuhuma zinazowakabili.

ASOMEWA KESI YA MAUAJI
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Christina Mbando, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Elizabeth Kaganda alimsomea mashtaka Lulu kwa kusema:
“Mnamo Aprili 7, mwaka huu, saa 7:00  usiku maeneo ya Sinza Vatican City jijini Dar, mtuhumiwa  Elizabeth Michael mwenye umri wa miaka 18, ulidaiwa kumuua Steven Kanumba.” Shitaka ambalo  Lulu hakutakiwa kulijibu.

AUKANA  UMRI WAKE
Hata hivyo, habari za ndani zilidai kuwa Lulu alinyoosha kidole kuashiria kutaka kumzungumza kitu, ndipo Hakimu Mbando alipompa nafasi ya kuzungumza.
Ilisemekana kuwa Lulu alisimama na kusema kuwa alikuwa akipinga umri wake ulioandikishwa kwenye kesi hiyo kwa kuwa  hajafikisha miaka 18  bali ana miaka 17 tu.
Hakimu Mbando alisema suala hilo litafuatiliwa baadaye ingawa mwendesha mashtaka wa kesi hiyo alisema mshitakiwa ni mtu maarufu na mambo yake mengi yanafahamika, hivyo hata umri wake unafahamika kuwa ni miaka 18 japo uchunguzi wa suala hilo utafanyiwa kazi.
Hakimu Mbando aliahirisha kesi hiyo mpaka Aprili 23, mwaka huu  ambapo mtuhumiwa atakapofikishwa kwa mara nyingine.

ASKARI WAPIGWA BUTWAA
Mtuhumiwa huyo alishushwa kizimbani  huku akiwa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa  katika Gereza la Segerea.
Usiri wa kumfikisha Lulu mahakamani ulisababisha hata maaskari wenye mamlaka ya kufanya taratibu za kimahakama kupigwa na butwaa walipomuona msanii huyo akiondolewa kwa kasi ya ajabu katika eneo la mahakama na kukimbizwa kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa Segerea.

TUJIKUMBUSHE
Asubuhi ya Jumamosi Aprili 7, mwaka huu, Lulu alikamatwa na askari wa Kituo cha Oysterbay baada ya kutokea kifo cha msanii Steven Charles Kusekwa Kanumba nyumbani kwake maeneo ya Vatican City Hotel, Sinza jijini Dar.
Habari zilisema kuwa Lulu alikuwa na Kanumba usiku wa tukio hilo na kulitokea mzozo kati yao walipokuwa chumbani kwa Kanumba.
Wakati Lulu akifikishwa mahakamani, Aprili 10, mwaka huu, Kanumba alizikwa katika makaburi ya Kinondoni, Dar.     

No comments